Breaking News

WAZIRI MKENDA AHAMASISHA WAHITIMU KUJITUMA , MAHAFALI DIT MWANZA

 

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Adolf Mkenda amesema mafanikio katika maisha hayategemei tu elimu ambayo wanafunzi wanaipata bali namna ambavyo watajituma.

Prof. Mkenda amesema hayo katika hotuba yake iliyosomwa leo na Kaimu Kamishna wa Elimu, Venance Manori katika mahafali ya nne ya Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam (DIT) Kampasi ya Mwanza.

"Maisha hayategemei tu elimu ya DIT kampasi ya Mwanza bali yanatokana pia na jitihada na mnavyotumia elimu hiyo, hivyo ninashauri kila mhitimu awe na dhana ya kujiajiri," amesema Prof. Mkenda kupitia hotuba hiyo.

Prof. Mkenda amesema serikali inaendelea kuboresha utendaji wa rasilimali watu katika taasisi za elimu ya ufundi na mafunzo ya ufundi stadi nchini kwa lengo la kuwezesha utoaji wa elimu.

Ameipongeza DIT kwa hatua ambayo imepiga kimaendeleo na kiteknolojia ambapo amesema kuwa mfumo na DIT Kampasi ya Mwanza kwa kuanzisha uhusiano na Chuo Kikuu cha Northampton cha nchini Uingereza na tayari MoU imewasilishwa katika taasisi hiyo na watumishi wawili wanasoma huko.

Aidha, amesema serikali inatambua DIT Kampasi ya Mwanza ina wajibu mkubwa katika kuchangia utekelezaji wa azma ya serikali ya kuchachua uchumi na maendeleo ya viwanda na kuitaka kampasi hiyo kuhakikisha lengo la kuwa Kitovu cha Taaluma na Mafunzo ya Teknolojia ya Ngozi inafikiwa.

Mkuu wa Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam,  Prof. Preksedis Ndomba amesema katika mahafali hayo kuna jumla ya sahitimu 64 (KE 18 na ME 46) na wahitimu wa Kampasi ya Mwanza ni wa  Stashahada ya Teknolojia ya Utengenezaji Bidhaa za Ngozi wanne na Sayansi na Teknolojia ya Maabara 21.

Wahitimu 39 ni kutoka Kampasi ya Dar es Salaam wa Stashahada na Shahada ya kwanza na wahitimu wa Kampasi ya Mwanza ni 25 (ME 14 na KE 11).  Prof. Ndomba amesema watunukiwa hao wamejengewa uwezo na ujuzi wa katika kutatua changamoto mbalimbali za kijamii mfano utengenezaji sanitaiza na vitu mbalimbali vya kimaabara pia viatu vya ngozi.

Nae Mwenyekiti wa Baraza la DIT,  Mhandisi Dkt. Richard Masika ameishukuru serikali ya Mhe. Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa mwaka huu wa fedha kiasi cha Sh bilionin 2.7 ambazo ni za awamu ya kwanza ya utekelezwaji wa mradi ya ukarabati wa miundombinu chakavu ya taasisi ukarabati ambao utagharimu jumla ya Sh bilioni 11.

Amewapongeza wahitimu kwa kumaliza safari yao hiyo kwa mafanikio, "hatua ambayo vijana wamepiga katika maisha yao ni kubwa na imeiva vizuri katika elimu ya darasani na mafunzo kwa vitendo.... hawa wote ni watendaji wazuri na wako tayari kuhudumia watanzania," amesema.

Katibu Tawala wa Wilaya ya Ilemela, Saidi Kitinga akimuwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, amesema uwekezaji mzuri katika nchi ni katika sayansi na teknolojia na kumleta mtoto kusoma DIT ni sehem sahihi.

"Mtoto akipata elimu hii inamuwezesha kujiajiri kwasababu tunakoelekea ajira za kuajiriwa hazitatutosha," amesema Kitinga na kuongeza kuwa nchi yenye uchumi imara ina amani na utuluvu.

Akisoma risala kwa niaba ya wahitimu wenzake, Msai Francis ameushukuru uongozi wa DIT kampasi ya Mwanza kutokana na elimu na ujuzi walioupata.

"Kwa ujuzi tulioupata tunajiamini na tunaweza kufanya kazi kama mafundi sanifu katika maeneo mbalimbali hususani viwandani, dhana ya Mafunzo kwa Vitendo (Teaching Factory) iliyoanzishwa kwenye taasisi hii imekuwa ya msaada kwetu na kuimarisha utendaji wetu," amesema.

Aidha, kutokana na changamoto ya baadhi ya wanafunzi wasio na uwezo kifedha kusitisha masomo yao kwa kukosa ada, wameiomba serikali kuangalia uwezekano kwa wanafunzi wa vyuo vya kati kupata mikopo.

No comments