AXIAN TELECOM PAMOJA NA ROSTAM AZIZI WAKAMILISHA MCHAKATO WA KUMILIKI KAMPUNI ZA MAWASILIANO ZA MILLICOM NCHINI TANZANIA
Muungano wa AXIAN Telecom na Rostam Aziz leo umetangaza kukamilika kwa mchakato wa umiliki wa kampuni iliyounganishwa ya MIC Tanzania Public Limited Company (Tigo na Zantel) katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Mchakato huu unaleta takribani wateja milioni 14 wa simu za mkononi kwa AXIAN Telecom na kuharakisha ukuaji wa kampuni hii barani Afrika ambapo kwa sasa imefika nchi nane katika bara hili.
Kwa kununuliwa kwa MIC Tanzania PLC, AXIAN Telecom inafungua ukurasa mpya katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Tunayo furaha kuanza safari hii ya kusisimua na wenzetu wa hapa (Tanzania) na ninaamini kwa pamoja tutafanikisha mambo makubwa yatakayoendelea kuongoza mapinduzi ya kidijitali hapa nchini. Tunatoa shukrani zetu kwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa kutusaidia kufanikisha mchakato huu, tunatarajia kuendelea kushirikiana kwa pamoja.
Hassanein Hirdjee, Mwenyekiti wa AXIAN Telecom.
Muungano wa AXIAN Telecom umeweka vipaumbele vinne (4) muhimu katika kutekeleza majukumu yake katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania:
· Kuendeleza mabadiliko ya kidijitali nchini kwa kutumia teknolojia za kisasa na kutoa huduma zinazowanufaisha mtumiaji mmoja mmoja na makampuni ya Kitanzania. Muungano huu una uwezo wa kutumia teknolojia za mtandao wa kasi na nyaya za chini ya ardhi ambazo zitaleta mawasiliano ya haraka kati ya Watanzania na kwingineko duniani.
· Kuongeza upatikanaji wa huduma nafuu za mawasiliano na kuongoza ujumuishwaji wa kidijitali kwa kuwekeza kikamilifu kwenye ujenzi wa miondombinu ya mawasiliano. Muungano huu unapanga kuimarisha upatikanaji na ubora wa mtandao hasa kupitia teknolojia ya 4G.
· Kuongeza kasi ya ujumuishwaji wa huduma za kifedha kwa njia ya simu za mkononi, kwa kuzingatia mafanikio ya huduma hizi kutoka kwenye kampuni zilizounganishwa ili kuendeleza zaidi huduma za kifedha kwa njia ya simu zinazolenga mahitaji ya wateja wa Tanzania. Umoja huo pia utahakikisha muungano huu unafaidika kupitia utaalamu wake wa kutoa huduma za kifedha za kiwango cha juu katika nchi zingine.
· Kukuza na kuendeleza vipaji. Muungano huo unakusudia kukuza maendeleo ya taaluma za wafanyakazi na kuweka mkazo mkubwa kwenye mafunzo, kubadilishana uzoefu na kushirikishana maarifa ya pamoja miongoni mwa wafanyakazi wa kampuni iliyounganishwa ya MIC Tanzania PLC.
Muungano huu unajumuisha AXIAN Telecom na Bw. Rostam Azizi, mtanzania mfanyabiashara na mjasiriamali ambaye ana taaluma ya muda mrefu kwenye sekta ya mawasiliano na amekuwa na mchango mkubwa kwenye maendeleo ya sekta hii hapa nchini Tanzania. Bw. Azizi, akiwa kama Mwenyekiti ajaye wa MIC Tanzania PLC, atatoa mwongozo wa kimkakati na usimamizi wa kampuni na mfumo mzima wa uendeshaji na upatikanaji wa huduma za mawasiliano kwa wadau wa sekta ya mawasiliano nchini Tanzania.
Tulipoanza safari yetu ya mawasiliano zaidi ya miaka ishirini iliyopita, suala kubwa lilikuwa kuunganisha watanzania kwenye huduma hii. Tulikuwa waanzilishi katika kujenga mtandao wa huduma za simu, hasa katika maeneo ya vijijini, ambapo kwa sasa Watanzania wenzangu wengi wanafurahia huduma hii. Tukitazama malengo ya pamoja na AXIAN Telecom, ni Dhahiri kuwa tutafanikiwa kuondoa vikwazo vinavyozuia upatikanaji wa huduma za kidigitali nchini kote, tukizingatia mahitaji muhimu kwa Watanzania na makampuni.
Rostam Azizi, Mwenyekitii MIC Tanzania PLC.
Ikitumia utaalamu wake hasa katika kusambaza teknolojia za hali ya juu kama vile mitandao ya 5G na kuanzisha huduma za kifedha kwa njia ya simu za mkononi zilizofanikiwa, AXIAN Telecom ina dhamira ya kuupa nguvu mfumo wa mawasiliano hapa Tanzania hasa katika kuhakikisha kuwa wateja wanapata huduma bora zaidi.
No comments