WANAFUNZI 30 WA DIT WALIOPELEKWA KUSOMA CHINA WAREJEA NCHINI
Na Mwandishi Wetu.
Dar es Salaam, Julai 12, 2026 – Wanafunzi 30 wa Idara ya Uhandisi Umeme kutoka Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam (DIT) waliokuwa nchini China kwa muhula mmoja wa masomo kupitia programu ya kubadilishana wanafunzi, wamerejea nchini wakiwa na ujuzi, uzoefu na mbinu mpya za kiteknolojia zinazotarajiwa kuongeza mchango wao katika maendeleo ya sekta ya teknolojia nchini.
Akizungumza katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) jijini Dar es Salaam wakati wa kuwapokea wanafunzi hao, Mkurugenzi wa Taaluma wa DIT, Dkt. Petro Pesha, amesema hatua hiyo ni sehemu ya mkakati wa taasisi hiyo wa kujenga ushirikiano na vyuo vikuu na taasisi mbalimbali za kimataifa ili kuwajengea wanafunzi uwezo wa kitaaluma na kiutendaji kupitia falsafa ya Teaching Factory, inayowapa nafasi ya kujifunza kwa vitendo sambamba na mazingira halisi ya kazi.Dkt. Pesha amesema DIT imekuwa ikipanua ushirikiano wake na taasisi mbalimbali za elimu ya juu ndani na nje ya Tanzania, ikiwemo Chuo cha Cho Ching nchini China ambako wanafunzi hao walisoma kwa muhula mmoja huku wakibadilishana maarifa, ubunifu na teknolojia na wenzao.
Ameeleza kuwa ushirikiano huo umeendelea kuzaa matunda, huku taasisi hiyo ikiwa tayari imepeleka pia wanafunzi wengine 15 katika chuo kingine nchini China kwa programu ya masomo ya miaka miwili.
"Malengo yetu ni kuwapa wanafunzi nafasi ya kujifunza teknolojia za kisasa kutoka kwenye nchi zilizoendelea kiteknolojia ili wanaporejea wawe sehemu ya kuleta mabadiliko chanya nchini. Aidha, tunaendelea kupanua ushirikiano wetu na taasisi nyingine duniani, ikiwemo mpango wa kuanzisha ushirikiano na chuo kutoka nchini Urusi," amesema Dkt. Pesha.
Kwa upande wake, Mkuu wa Idara ya Uhandisi Umeme DIT, Dkt. Mwaka Ismail Juma, amesema wanafunzi hao wamepata mafunzo ya vitendo yanayowawezesha kutekeleza teknolojia mbalimbali kwa ufanisi badala ya kutegemea nadharia pekee.
Amesema matarajio ya DIT ni kuona wanafunzi hao wanatumia maarifa waliyoyapata kubuni teknolojia na suluhisho zitakazosaidia kutatua changamoto mbalimbali zinazoikabili jamii na taifa kwa ujumla.
Dkt. Mwaka ameongeza kuwa walimu wa DIT pia watanufaika na programu hiyo kwa kukutana na wanafunzi hao ili kujifunza mbinu za ufundishaji, matumizi ya teknolojia na mifumo ya elimu waliyoishuhudia nchini China, hatua itakayosaidia kuendelea kuboresha ubora wa elimu inayotolewa chuoni hapo.
Wakizungumza baada ya kuwasili nchini, wanafunzi Grace Marwa na Anaph Zuberi wameishukuru DIT kwa kuwapatia fursa hiyo adimu wakisema imewapa maarifa mapya, uzoefu wa kimataifa na uwezo mkubwa zaidi wa kutumia teknolojia katika kutatua changamoto za maisha halisi.
Wamesema wangependa kuona wanafunzi wengi zaidi wakinufaika na programu hiyo ili Tanzania iendelee kuzalisha wahandisi wenye weledi, ubunifu na uwezo wa kushindana katika soko la ajira la kimataifa.
Naye mzazi wa mmoja wa wanafunzi hao, Amina Lupyana, ameipongeza DIT kwa kuendelea kufungua milango ya fursa za kimataifa kwa wanafunzi wake.
Amesema programu hiyo imeongeza thamani kubwa katika safari ya elimu ya watoto wao na kuwataka wazazi wengine kujiamini na kuwapeleka watoto wao DIT ili wanufaike na mazingira bora ya kujifunza pamoja na fursa mbalimbali za kimataifa zinazotolewa na taasisi hiyo.
Mpango huo unaendelea kudhihirisha dhamira ya DIT ya kuzalisha wahitimu wenye ujuzi wa kisasa, uwezo wa kufanya kazi kwa vitendo na ushindani wa kimataifa, sambamba na kuunga mkono jitihada za Tanzania za kukuza uchumi unaotegemea sayansi, teknolojia na ubunifu.












No comments