Breaking News

BUNIFU ZA WANAFUNZI DIT ZAWAVUTIA WENGI MAONESHO YA SABASABA 2026.

Na Mwandishi Wetu.

Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam (DIT) imeendelea kuthibitisha kuwa ni kitovu cha ubunifu na teknolojia nchini kupitia ushiriki wake katika Maonesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (SABASABA) 2026, ambapo bunifu mbalimbali zilizobuniwa na wanafunzi wa taasisi hiyo zimeendelea kuvutia maelfu ya wageni wanaotembelea banda la DIT kila siku.

Bunifu hizo hazioneshi tu uwezo wa kitaaluma wa wanafunzi wa DIT, bali pia zinaakisi namna taasisi hiyo inavyoandaa wataalamu wenye uwezo wa kubuni teknolojia zinazotoa suluhisho kwa changamoto halisi zinazoikabili jamii katika sekta za afya, usafiri, nishati, viwanda na ujasiriamali.

Miongoni mwa bunifu zinazovutia zaidi ni jiko la kisasa la kupikia (Improved Gasifier Cook Stove) lililobuniwa na mwanafunzi Huruma Daison Msongwe. Jiko hilo limeboreshwa kwa matumizi yenye ufanisi mkubwa wa nishati, likipunguza matumizi ya mafuta au kuni, gharama za upishi pamoja na kulinda mazingira.



Katika sekta ya usafiri, mwanafunzi Oliva Felix Sangawe amewasilisha mfumo wa BRT Tracking System, teknolojia inayowaruhusu abiria wa mabasi yaendayo haraka (Mwendokasi) kufuatilia mahali basi lilipo kwa wakati halisi pamoja na kujua muda litakaofika katika kituo husika. Mfumo huo unatarajiwa kuwasaidia wananchi kupanga safari zao kwa ufanisi na kupunguza muda wa kusubiri vituoni.

Sekta ya afya nayo imewakilishwa na mwanafunzi Hamida Dhamir, aliyebuni Orthotic Equipment, kifaa kinachowasaidia watoto waliopooza kutokana na ajali, kiharusi au magonjwa mengine kurejesha uwezo wa kutembea. Mbali na kutengeneza kifaa hicho, timu hiyo pia hutoa ushauri wa kitaalamu kuhusu matumizi sahihi ya vifaa hivyo.



Katika kuboresha huduma za afya, mwanafunzi Rahma Kahindi ameleta bunifu ya Smart Movable Wound Dressing Set, kifaa kinachorahisisha utoaji wa huduma za usafishaji wa vidonda, hususan kwa wagonjwa wa kisukari wenye vidonda vya miguu, hivyo kuongeza ufanisi na usalama katika utoaji wa huduma.


Kwa upande wa ubunifu wa viwandani, mwanafunzi Arnold Kimaro ameibuka na kiatu cha kisasa aina ya Sandal chenye mikanda inayoweza kubadilishwa. Ubunifu huo humwezesha mtumiaji kubadili muonekano wa kiatu kulingana na mavazi au mahitaji yake bila kulazimika kumiliki jozi nyingi za viatu, jambo linalopunguza gharama na kuongeza urahisi hasa kwa wasafiri.

Akizungumza katika maonesho hayo, Mkuu wa Idara ya Ushirikiano wa Viwanda na Muongozo wa Kazi wa DIT, Mhandisi Hafidh Yusuf, amesema bunifu zinazowasilishwa na wanafunzi wa DIT zinaonesha kiwango kikubwa cha ubunifu na maarifa yanayotolewa na taasisi hiyo, huku zikitoa majawabu ya changamoto mbalimbali zinazowakabili Watanzania.

Amesema DIT itaendelea kuwekeza katika elimu ya vitendo, utafiti na ubunifu ili kuzalisha wahandisi na wataalamu wenye uwezo wa kubuni teknolojia zinazochochea maendeleo ya viwanda, huduma za jamii na uchumi wa taifa.

"Tunawakaribisha wananchi wote kutembelea banda la DIT katika Maonesho ya SABASABA 2026 ili kujionea bunifu mbalimbali zilizotengenezwa na wanafunzi wetu, kufahamu teknolojia zinazotoa suluhisho kwa changamoto za jamii, pamoja na kupata taarifa kuhusu programu za masomo, tafiti na fursa mbalimbali zinazotolewa na Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam," amesema Eng. Hafidh Yusuf.



Bunifu hizi ni sehemu ya mafanikio ya DIT katika kuandaa wataalamu wenye uwezo wa kubadili mawazo kuwa bidhaa, huduma na teknolojia zenye tija kwa jamii. Kupitia mazingira bora ya kujifunzia, maabara za kisasa na ushirikiano wake na sekta ya viwanda, DIT imeendelea kujijengea heshima kama taasisi inayoongoza katika kukuza ubunifu unaochochea maendeleo ya Tanzania.

Wageni wanaoendelea kutembelea banda la DIT katika SABASABA 2026 wamekuwa wakionesha kuvutiwa na ubora wa bunifu hizo, huku wengi wakieleza kuwa zinaonesha uwezo mkubwa wa vijana wa Kitanzania katika kubuni teknolojia zinazoweza kushindana katika soko la kitaifa na kimataifa.









No comments