Breaking News

TBS YAENDELEA KUINUA SEKTA YA UOKAJI NCHINI KUPITIA MAFUNZO YA VIWANGO NA UBORA

Na Mwandishi Wetu.

Katika jitihada za kuendelea kulinda afya za watumiaji na kukuza uchumi wa wajasiriamali nchini, Shirika la Viwango Tanzania (TBS) limeendelea kuonesha dhamira yake ya dhati kwa kutoa mafunzo maalumu kwa wadau wa sekta ya uokaji kuhusu umuhimu wa kuzingatia viwango vya ubora na usalama wa chakula.

Mafunzo hayo yaliyofanyika jijini Dar es Salaam yamewakutanisha wazalishaji mbalimbali wa mikate, maandazi na bidhaa nyingine za uokaji, yakilenga kuwajengea uwezo wa uzalishaji bora unaokidhi viwango vya kitaifa na kimataifa.

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo, Mkurugenzi wa TBS, Dkt. Ashura Katunzi amesema serikali kupitia TBS itaendelea kuweka mazingira wezeshi kwa wafanyabiashara ili waweze kuzalisha bidhaa salama na zenye ubora unaokubalika sokoni.


Amesema sekta ya uokaji ina mchango mkubwa katika uchumi wa wananchi na ajira, hivyo kuna umuhimu mkubwa kwa wazalishaji kuhakikisha wanazingatia usafi wa mazingira, matumizi sahihi ya malighafi pamoja na taratibu bora za uzalishaji na usafirishaji wa bidhaa za chakula.

“Tunataka kuona bidhaa zinazotengenezwa na wajasiriamali wetu zinakuwa salama kwa mlaji na zenye uwezo wa kushindana katika masoko mbalimbali. Elimu hii ni muhimu katika kujenga uchumi imara unaozingatia ubora,” amesema Dkt. Katunzi.

Kwa upande wake, Meneja wa TBS Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Bi. Noor Meghji amesema mafunzo hayo ni sehemu ya mkakati wa TBS wa kuendelea kuwafikia wajasiriamali wa sekta mbalimbali ili kuwajengea uelewa kuhusu viwango na ubora wa bidhaa.

Amesema sekta ya uokaji imeendelea kukua kwa kasi na kuwa chanzo kikubwa cha kipato kwa wananchi wengi, hivyo ni muhimu kuhakikisha bidhaa zinazozalishwa zinakidhi matakwa ya afya na usalama wa chakula.

Bi. Meghji ameongeza kuwa TBS itaendelea kutoa elimu kwa wafanyabiashara ili kuwasaidia kuongeza ushindani wa bidhaa zao sokoni sambamba na kujenga imani kwa watumiaji.

Baadhi ya washiriki wa mafunzo hayo wameipongeza TBS kwa kuendelea kutoa elimu inayowasaidia kuboresha biashara zao, wakisema maarifa waliyopata yatawasaidia kuongeza ubora wa bidhaa, kuimarisha usafi pamoja na kutumia mbinu bora za ufungashaji na uhifadhi wa bidhaa za uokaji.

Wamesema mafunzo hayo yamekuwa chachu ya mabadiliko katika biashara zao kwani yamewawezesha kuelewa kwa kina namna ya kuzalisha bidhaa salama zinazokubalika na walaji.

Hatua ya TBS kuendelea kutoa mafunzo kwa wadau wa sekta mbalimbali inaonesha namna ambavyo shirika hilo linaendelea kuwa nguzo muhimu katika kuhakikisha bidhaa zinazozalishwa nchini zinakuwa na ubora unaolinda afya za wananchi na kuongeza ushindani wa bidhaa za Tanzania ndani na nje ya nchi.






No comments