Breaking News

TBS WATOA ELIMU YA VIWANGO KWA WANAFUNZI WABUNIFU CHUO CHA CBE

Na Mwandishi Wetu.

Dar es Salaam, Mei 29, 2026 — Shirika la Viwango Tanzania (TBS) limeendelea kudhihirisha dhamira yake ya kukuza ubunifu na maendeleo ya viwanda nchini baada ya kushiriki katika Maonesho ya Fursa za Kazi na Ubunifu kwa Vijana (Career Fair 2026) yaliyofanyika katika Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE).

Maonesho hayo yaliyobeba kauli mbiu isemayo “Ubunifu na Ujuzi kwa Vijana ni Msingi wa Ukuaji wa Biashara na Viwanda Tanzania”, yaliwakutanisha wanafunzi, wahitimu wa zamani (Alumni), wabunifu pamoja na wadau mbalimbali wa maendeleo ya viwanda na biashara nchini.

Mgeni rasmi katika maonesho hayo alikuwa Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Dennis Londo, ambaye alitembelea mabanda mbalimbali na kujionea kazi za ubunifu zinazofanywa na vijana wa Kitanzania.


Katika maonesho hayo, TBS ilitumia fursa hiyo kutoa elimu kwa wanafunzi na wabunifu kuhusu umuhimu wa kuzingatia viwango vya ubora katika bidhaa wanazozalisha, sambamba na kuwaelekeza namna ya kupata Alama ya Ubora ya TBS ili kuwaongezea ushindani wa bidhaa zao katika soko la ndani na kimataifa.

Akizungumza katika banda la TBS, Eng. Angela Charles ambaye ni Afisa Metrolojia wa TBS, alisema vijana wengi wana vipaji na ubunifu mkubwa lakini bado wanahitaji mwongozo wa kitaalamu kuhusu ubora na vipimo sahihi vya bidhaa zao ili waweze kuzalisha bidhaa zinazokidhi mahitaji ya soko.

Alieleza kuwa ushiriki wa TBS katika maonesho hayo ni sehemu ya mkakati wa shirika hilo kuwafikia vijana moja kwa moja na kuwajengea uelewa kuhusu taratibu za ubora, upimaji pamoja na faida za kupata ithibati ya viwango kwa bidhaa zao.

“Tunataka vijana waelewe kuwa ubunifu pekee hautoshi, bali ubora ndio unaoongeza thamani ya bidhaa na kuipa nafasi ya kuaminika sokoni,” alisema Eng. Angela.

Kwa upande wake, mmoja wa wanafunzi wabunifu walioshiriki maoneshoni hapo, Omary Kisoma ambaye ni mbunifu wa sabuni ya maji, alisema amefaidika kwa kiasi kikubwa na elimu aliyopata kutoka TBS kuhusu hatua za kupata Alama ya Ubora kwa bidhaa yake.

Omary alisema awali alikuwa akihofia kuwa mchakato huo ungekuwa mgumu na wenye gharama kubwa, lakini baada ya kupata elimu kutoka kwa wataalamu wa TBS ameona kuwa utaratibu huo ni rahisi na wenye manufaa makubwa kwa wajasiriamali wanaotaka kukuza biashara zao.

“Nimejifunza namna ya kuboresha bidhaa yangu na hatua za kupata alama ya ubora ili niweze kuuza katika masoko makubwa zaidi hata nje ya nchi,” alisema Omary kwa furaha.

Ushiriki wa TBS katika Maonesho ya Fursa za Kazi na Ubunifu CBE 2026 umeonekana kuwa chachu muhimu kwa vijana wabunifu nchini, huku ukiendelea kuonesha namna ambavyo taasisi hiyo imejikita katika kuunga mkono ajenda ya serikali ya kujenga uchumi wa viwanda kupitia vijana wenye maarifa, ubunifu na bidhaa zenye ubora unaokubalika kitaifa na kimataifa.







No comments