Breaking News

KONGAMANO LA UWEKEZAJI AFRIKA MASHARIKI KUTIKISA

 

Makamu Mwenyekiti wa mtandao wa Umoja wa Wanachama watoa Huduma za Kifedha kwa njia ya Teknolojia ( TAFINA) Bw. Reuben Mwatosya ( katikati ) akizungumza na waandishi wa Habari ( hawapo pichani ) kuhusu maandalizi kuelekea Kongamano kubwa la Uwekezaji la Afrika Mashariki (EAIF) 2024, linalotarajiwa kufanyika Septemba 12 na 13, 2024, katika Hoteli ya Serena jijini Dar es Salaam, kulia ni Bwn. Shadrack Kamenya Katibu Mkuu wa TAFINA na kushoto ni Bi. Juliet Kiluwa.

Na Adery Masta.

Wawekezaji zaidi ya 10 kutoka nchi mbalimbali za Afrika  wanatarajia kushiriki katika Kongamano kubwa la wafanyabiashara Afrika Mashariki “East Africa Investment Forum’ lenye lengo la kuunganisha wafanyabiashara hususani watoa huduma za kifedha kwa njia ya mtandao kutoka nchi za Afrika Mashariki na Kati.

Akizungumza na waandishi Leo  Septemba , 04 , 2024 jijini Dar es Salaam, Makamu Mwenyekiti wa mtandao wa Umoja wa Wanachana watoa Huduma za Kifedha kwa njia ya Teknolojia ( TAFINA), Reuben Mwatosya alisema Kongamano hilo, lililoandaliwa kwa ushirikiano na vyama vikuu vya FINTECH kutoka Kenya, Uganda, Rwanda, Burundi, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, na Tanzania, litafanyika Septemba 12 na 13, 2024, jijini Dar es Salaam.

“Kongamano hili ni muhimu kwanza kuwaleta watu pamoja ambao wataweza kushirikiana katika sehemu mbalimbali, hivyo sasa ni wakati wa kuwaleta watu hawa pamoja kujadiliana ni vipi wataweza kufanya kazi pamoja, kujifunza ni namna gani Teknolojia hizi mfano AI zitaweza kusaidia kuondoa changamoto mbalimbali”

Pia alisema katika kongamano hilo, kutakuwa na wageni zaidi ya 300 wanaokuja kuwakilisha makampuni na Mashirika mbalimbali kutoka Duniani kote.

“Wageni watakaokuwepo ni zaidi ya 300 kutoka nchi mbalimbali na tunadhani mkutano huu lengo lake ni kuleta chachu ya kuleta wawekezaji Tanzania”

Alisema wanaendelea kupokea wageni na watu ambao wanataka kuja kushiriki katika kongamano hilo wakishirikiana na wadau ambao tayari wanafanya nao kazi kwa sasa wakiwemo Selcom, TALA, n.k

Kwa upande wake, Katibu Mkuu -TAFINA, Shadrack Kamenya alisema katika kongamano hilo, kutakua na watoa mada mbalimbali ambazo zimegawanyika katika makundi mbalimbali ikiwemo kisera, uwekezaji, na mashirikiano baina ya watoa huduma .

Kamenya alisema maeneo ambayo wataenda kuyaangazia katika mada hizo ni eneo la uwekezaji, sera, matumizi sahihi ya Teknolojia n.k 

“Hili litakua ni eneo mahususi hasa kwa serikali na wadau wengine kuona ni kitu gani kinafanyika nje ya nchi au sokoni na kuweza kurahisisha utoaji wa huduma na tunaamini kwamba kumekuwa na maendeleo siku za karibuni katika sekta ya kifedha”

“Tunaamini kwamba kuwaleta watoa huduma wengine na mashirikisho mengine tutaweza kujifunza zaidi nini kinafanyika lakini pia tutaanzisha mazungumzo na tutazidi kutengeneza wepesi wa kuweza kuvutia zaidi uwekezaji Tanzania na kuboresha sekta ya fedha” alisema 

Katika kongamano hilo, mgeni rasmi anatarajiwa kutoka Benki kuu ya Tanzania ambapo ataambatana na wageni wengine .

No comments