Breaking News

Benki ya Absa yaendeleza udhamini wake Absa Dar City Marathon

Mkuu wa Masoko na Mawasiliano wa Benki ya Absa Tanzania, Bwana Aron Luhanga (wa pili kushoto) akionyesha fulana zitakazovaliwa siku ya mbio za Absa Dar City Marathon wakati wa hafla ya uzinduzi wa mbio hizo jijini Dar es Salaam jana, zinazotarajiwa kufanyika Mei 5 mwaka huu, jijini Dar es Salaam. Kutoka kushoto ni Ofisa Masoko wa Hill Water, Sylvia Shoo, Mkuu wa Kitengo cha Habari wa Klabu ya The Runners, waandaaji wa Absa Dar City Marathon, Godfrey Mwangungulu, Meneja wa Bima Kibenki wa Alliance Life Assurance, Juma Patrice na Meneja Bima Binafsi, Jumanne Muruga.

BENKI ya Absa Tanzania imeendeleza udhamini wake kwa mwaka wa nne mfululizo katika mbio za Absa Dar City Marathon , ikilenga kuifanya Tanzania kuwa Taifa lenye watu wenye afya njema.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa mbio za Absa Dar City Marathon 2024, Mkuu wa Masoko na Mawasiliano wa benki hiyo, Bwana Aron Luhanga alisema afya njema ni mtaji namba moja katika maendeleo ya Taifa la Tanzania na wanaokimbia wanajenga Afya.

Alisema lengo lingine kuu la Absa Dar City Marathon ni mapato yatayakayopatikana katika mbio hizo kuelekezwa katika shughuli za kijamii Kwa kununua vifaa vitakavyosaidia wodi ya wanawake katika hospitali ya Mnazi Mmoja jijini Dar es Salaam.

Pamoja na hayo kama kauli mbiu ya mbio hizi isemayo ‘Kata Mtaa, Ujue Jiji’ sisi kama Absa Bank, tukiwa na Matawi ya kibenki hapa jijini, tunajisikia fahari kusapoti mbio hizi zenye lengo pia la kutangaza vivutio vya utalii vilivyomo katika jiji letu."

Kauli yetu ya Absa inasema ‘Story Yako ina Thamani’ hivyo tunaamini kuwa ukienda kukimbia unaandika Story Yako, ukienda kusaidia jamii, unaandika Story Yako, nasi kama Absa, Story Yako Ina thamani sana kwetu”, alisema Bwana Luhanga.

Awali akizungumza katika hafla hiyo, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano wa The Runners Club, Bwana Godfrey Mwangungulu alisema mbio za mwaka huu zinazofanyika chini ya udhamini mkubwa wa Benki ya Absa Tanzania zitashirikisha mbio za Kilomita, 21, 10 na Kilomita tano.

Absa Dar City Marathon ya mwaka huu inayotarajiwa kufanyika Mei 5 mwaka huu ikianzia katika Viwanja vya Mnazi Mmoja, ni zaidi ya mbio, ni zaidi ya sherehe, ni kilele cha sherehe za mbio zote zinazoendelea kufanyika hapa nchini."

Tumefanya mbio hizi kwa miaka mitatu mfululizo, mwaka huu tunataka kuzifanya Kwa mafanikio zaidi, tunatarajia zaidi ya wakimbiaji 3000 kushiriki, tunawashukuru sana wadhamini wetu wakuu, Benki ya Absa pamoja na wadhamini wengine”, alisema Bwana Mwangungulu.

Mbali na Benki ya Absa kama mdhamini mkuu, wadhamini wengine ni Kampuni ya Alliance Life Assurance, Hill Water, Kilimanjaro Milk na Kampuni ya Garda Security.
Mkuu wa Masoko na Mawasiliano wa Benki ya Absa Tanzania, Bwana Aron Luhanga (wa tatu kushoto), Mkuu wa Kitengo cha Mawasilino wa The Runners Club, Bwana Godfrey Mwangungulu (kushoto kwa Aron), pamoja na wawakilishi wa wadhamini wengine, wakionyesha fulana na vitu vingine vitakavyotumika wakati wa mbio za Absa Dar City Marathon, jijini Dar es Salaam Mei 5 mwaka huu, zikianzia katika Viwanja vya Mnazi Mmoja. Hafla hiyo ilifanyika jijini humo jana.

No comments