Waziri Ndugulile:Tunaandaa sheria ya faragha kulinda taarifa za mtumiaji
Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, TEHAMA Faustine Ndugulile akizungumza na waandishi wa habari wakati wa mdahalo wa wadau wa sekta ya Tehama
Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Faustine Ndugulile amesema katika kutengeneza mazingira rafiki na wezeshi ya sekta ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano TEHAMA, anakusudia kutunga sheria ya faragha.
Pia ametoa wito kwa wadau kupeleka mawazo, maoni au ushauri namna ya kuboresha sekta hiyo nchini.
Ndugulile ametoa kauli hiyo juzi katika mdahalo wa wadau wa sekta ya Tehama ambao pamoja na mambo mengine ulilenga kujadili changamoto na suluhisho kuhusu sekta ya Mawasiliano na tekbnolojia nchini.
Akizungumza katika mdahalo huo uliokuwa na mada kuu kuhusu mapinduzi ya nne ya viwanda kwa uchumi wa dijitali wa ushindani, Dk. Ndugulile alisema wizara yake inakwenda kufanya marekebisho ya sheria mbalimbali za sekta hiyo.
"Tunaenda kupitia sheria na kanuni zetu na tutafanya mabadiliko ili kukidhi mazingira ya sasa, tunakusudia kutunga sheria ya faragha na kulinda taarifa za mtumiaji(Data Privacy and Protection).
"Nimekuwa msikilizaji wa mdahalo kwa kweli tumepata mengi kutoka kwa wadau na kama serikali tunaenda kuyafanyia kazi kwa haraka.
"Muda wowote wadau leteni mawazo, maoni na ushauri ni namna gani tuboreshe na tusonge mbele uzuri hata mitandaoni nipo ukienda Twitter utanipata, Instagram nipo na twitter nipo na uzuri kwa sasa inapatikana vizuri na mnaipata vizuri pia.
"Kuhusu TCRA nimetoa maelekezo tayari wasifanye kazi kama polisi bali kama mlezi, mimi sio muumini wa faini kubwa kubwa lazima tubadilike na tumeanza kubadilika, alisema.
Akizungumza kwenye mkutano huo Dk Bello Moussa, Mkuu wa Ubunifu na Mikakati ya TEHAMA Huawei Kusini mwa Afrika alisema: "Mapinduzi ya Nne ya Viwanda yanakuja na maendeleo ya kiteknolojia yanaendesha maendeleo ya ulimwengu, ni wakati mzuri sasa kwa Tanzania kutosalia nyuma, bali kuungana na ulimwengu wote kwa kufanya kazi kwenye maeneo ambayo yataharakisha Mapinduzi ya Nne ya Viwanda Tanzania katika Miaka 5 ijayo ”
Alitaja maeneo hayo ambayo ni pamoja na mpango wa kitaifa wa TEHAMA kwa uchumi wa kidigiti, mkongo wa taifa wenye kasi zaidi, ufikiwaji wa huduma ya internet maeneo ya vijijini na wataalamu wa wataalam wa TEHAMA.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Baraza la Taifa la Biashara (TNBC), Dk. Godwill Wanga alisema Tehama imeleta matokeo chanya katika sekta mbalimbali ikiwamo kupunguza gharama za uzalishaji, kuongezeka uwekezaji na ukuaji wa uchumi wa nchi.
No comments