Swissport yatoa msaada wa machine mbili zenye thamani ya Sh.Milioni 12.6 katika Hospitali ya Temeke
Kaimu Mganga Mkuu wa hospitali ya Wilaya ya Temeke, Dk. Serafini .K. Patrice (kushoto) akipokea moja ya mashine zenye thamani ya shilingi milioni 12.6 ijulikanayo kwa jina la Patient Monitor inayofuatilia muenendo wa afya ya mgonjwa kutoka kwa Mkurugenzi wa kampuni ya Swissport Tanzania, Nd. Yassin Mrisho.
KAMPUNI ya kuhudumia mashirika ya ndege, abiria na mizigo katika viwanja vya ndege ya Swissport imetoa msaada wa mashine mbili za kufatilia afya ya mgonjwa anapokuwa katika hali isiyo ya kawaida, zenye thamani ya Sh. Milioni 12.6 kwa Hospitali ya Wilaya ya Temeke.
Akizungumza jijini Dar es Salaam jana wakati wa kukabidhi msaada huo hospitalini hapo, Ofisa Mtendaji Mkuu wa kampuni hiyo, Mrisho Yassin alisema wamesukumwa kutoa msaada huo ili kuweza kuokoa maisha ya mama na mtoto wanaofika katika hospitali hiyo kupata huduma.
Alisema kampuni yao imekuwa na sera ya kusaidia jamii hasa katika maeneo ya afya na elimu hivyo wakati huu wa kumaliza mwaka wameamua kutoa msaada huo ambao utakwenda kupunguza baadhi ya changamoto zilizokuwa zinaikabili hospitali hiyo.
“Tumekuja katika hopsitali hii kwa sababu tunataka kuisaidia jamii hivyo mashine hizi mbili ambazo kwa jina la kitaalamu zinajulikana kama Patient Monitor zitakwenda kusaidia watoto ambao mara nyingi si rahisi kutambua wanaumwa nini pia itawasaidia kinamama,” alisema Yassin na kuongeza.
“Tutaendelea kushirikiana zaidi na hospitali hii ili kuweza kutatua baadhi ya changamoto zingine zilizopo, lakini pia jambo hilo limefungua mlango kwa wadau wengine kujitokeza kusaidia,” alisema.
Naye Kaimu Mganga Mkuu wa hospitali hiyo, Dk. Serafini Patrice alisema pamoja na kupokea msaada huo bado wanakabiliwa na changamoto ya ukosefu wa chumba cha wagonjwa mahututi (ICU) pamoja na wod, hivyo wanawaomba wadau wengine kujitokeza kuweza kusaidia.
“Licha ya kwamba Serikali imekuwa ikijitahidi kwa kiasi kikubwa kuisaidia hospitali hiyo ambayo inamadaktari bingwa zaidi ya 10, lakini bado peke yake haiwezi kumaliza changamoto zilizopo katika hospitali hii hivyo basi tunawaomba wadau wengine wajitokeza kusaidia,” alisema.
Aidha alisema hospitali hiyo imekuwa ikiwahudumia wagonjwa zaidi ya Milioni 1.6 ila magonjwa waliomengi ni yale ya kinamama pamoja na ya upasuaji wa mifupa.
No comments