Breaking News

LSF wadau kushirikiana kukomesha Ukatili wa Kijinsia Tanzania

Mtendaji Mkuu wa Shirika la Legal Services Facility (LSF) akiongea wakati wa uzinduzi wa Siku 16 za Kupinga Ukatili wa Kijinsia, maadhimisho yaliyofanyika jijini Dodoma jana. (Picha na Mpiga Picha Wetu).

Na Mwandishi Wetu
Shirika la Legal Services Facility (LSF) limetoa wito kwa wadau wa haki za binadamu kuunganisha nguvu na kushirikiana na Serikali katika kupiga vita na kutokomeza ukatili wa kijinsia nchini Tanzania.
“Inabidi tuunganishe nguvu ili tuweze kushinda vita hii. Hatuwezi kufanikiwa kutokomeza ukatili wa kijinsia bila kuunganisha nguvu zetu. Ushirikiano ni muhimu sana,” anasema Afisa Mkurugenzi Mkuu wa LSF, Bi. Lulu Ng’wanakilala, wakati wa uzinduzi wa siku 16 za Kupinga Ukatili wa Kijinsia yaliyofanyika jijini Dodoma. Mgeni Rasmi wa Uzinduzi wa maadhimisho haya yenye Kauli Mbiu “Kizazi chenye usawa, simama dhidi ya ubakaji” alikuwa Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Mhe. Ummy Ally Mwalimu.
Amesema LSF imekuwa mstari wa mbele katika vita dhidi ukatili za kijinsia, na mara kwa mara “tumekuwa tunashiriki katika maadhimisho ya siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia.”
Kwa mujibu wa Ng’wanakilala, kila mwaka “LSF tumekuwa tunashirikiana na wadau mbalimbali, ikiwa ni pamoja na vitengo mbalimbali vya serikali kuandaa maadhimisho haya yenye lengo la kutokomeza vitendo vya kikatili vinavyovunja haki na usawa wa binadamu kwa ujumla.”
Kwa mujibu wa Mkurugenzi huyo, LSF imefanya kazi kubwa kutokomeza ukatili wa kijinsia, kupitia wasaidizi wa kisheria wanaofanya kazi katika vijiji na kata mbalimbali nchini nzima.
“Takwimu zetu zinaonesha  kesi za ukatili wa kijinsia zilizoripotiwa kwa watoa huduma wetu wa msaada wa kisheria 5,226 kati ya hizo wanawake ni 3,447 na wanaume 1,779. Hadi Septemba mwaka huu, kesi hizi zilikuwa zimefika 7,483, ambapo wanaume ni 3,357 na wanawake 4,126. Kesi hizi za ukatili wa kijinsia ni sawa na asilimia 7 ya idadi ya kesi tunazozishughulikia kwa mwaka ambazo jumla yake ni 76, 513,” amesema Mtendaji wa LSF.
“Kesi za ubakaji zilizoripotiwa kwa kwa watoa huduma wa msaada wa kisheria zinafikishwa katika vyombo mbalimbali ikiwemo polisi hadi Septemba Mwaka huu ni 94, kati ya hizo wanawake ni 88 na wanaume 6. Hii inaonesha jinsi gani wanawake wanavyoathirika kwa kiasi kikubwa na ukatili wa kijinsia,” aliongeza.
Alisema LSF itaendelea kushirikiana na Serikali na wadau wengine katika kutokomeza vitendo vya ukatili wa kijinsia, na kuhakikisha kuwa haki za wanawake, watoto wa kike na watu maskini zinalindwa. “Lengo kuu ni kuisaidia Serikali ifikie malengo yake ya kuijenga Tanzania yenye amani, usawa, haki na maendeleo hasa kwa wanyonge.”
LSF ni shirika lisilo la kiserikali lililosajiliwa mwaka 2011 kwa lengo la kusaidia kuhakikisha haki sawa inapatikana kwa watu wote, hasa kwa wanawake kupitia uwezeshaji wa kisheria. Katika utekelezaji wa miradi yake, inatoa ruzuku kwa mashirika zaidi ya 200 yanayotoa huduma za msaada wa kisheria Tanzania Bara na Zanzibar.

No comments