Breaking News

Kampuni ya bima ya UAP yashauriwa kuendelea kuwa karibu na wateja wake


Kiongozi wa tawi la Kampuni ya UAP Zanzibar, Bi. Faridah Saleh akisalimia wateja waliokuja kujumuika na kampuni hiyo. Kushoto kwake ni Mkuu wa kitengo cha Uendelezaji Biashara na Masoko Bw. Jabir Kigoda baada ya kutoa hotuba ya kuwakaribisha wageni waalikwa pamoja na wateja wa kampuni hiyo ndani ya Hotel Verde Zanzibar.
Mkuu wa kitengo cha Uendelezaji Biashara na Masoko Bw. Jabir Kigoda akizungumza na wageni waalikwa pamoja na wateja baada ya kufuturu nao pamoja katika ghafla iliyoandaliwa ndani ya Hotel Verde Zanzibar
Naibu Kamishina wa Bima Bi. Khadija Said akiwasilisha hotuba yake katika hafla hiyo.
Menejimenti ya kampuni ya bima ya UAP ikiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya mawakala wa kampuni hiyo waliopo Zanzibar.

Kampuni ya bima ya UAP imeshauriwa kuendeleza utaratibu wake wa kuwa karibu na wateja wake wanaopatikana Zanzibar.

Hayo yalisemwa hivi karibuni na Waziri wa Fedha na Mipango wa Zanzibar, Mh. Mohammed Ramia Abdiwawa wakati wa futari ya pamoja iliyoandaliwa na kampuni hiyo ya bima ndani ya HotelVerde mjini hapo.

‘Tunaishukuru kampuni hii kwa kuona umuhimu wa kuandaa futari kwa ajili ya wateja wake kwa lengo la kuweza kudumisha mshikamano uliopo baina yao. Na ningeomba kwa hili niwapigie debe kwani ni kampuni ambayo imekuwa na utamaduni huu kila mwaka na ninawaomba waendelee hivi hivi, alisema Mhe.Ramia

Nae mkuu wa kitengo cha uendelezaji biashara na masoko Bw. Jabir Kigoda alielezea umuhimu wa soko la Zanzibar kwa kampuni ya bima ya UAP, na pia kusema utaratibu huo wa kuwa karibu na wateja utaendelezwa kwani kwao wateja ni sehemu ya familia ya kampuni hiyo. Hivyo basi wanastahili kukutana ili kudumisha familia yao hiyo kubwa inayozidi kukua siku hadi siku.

Pamoja na hayo, Mkuu wa kitengo cha fedha ambae pia ni Kaimu Mkurugenzi wa kampuni hiyo Bw, Nelson Rwihula aliishukuru mamlaka ya bima Tanzania kwa kuendelea kuliendesha vizuri soko la bima hapa nchini.

Ghafla hiyo pia ilihudhuriwa na Naibu Kamishina wa Bima Tanzania Bi. Khadija Said. Naibu Kamishina pia aliipongeza UAP kwa utaratibu huu na kuitaka pia iweze kushiriki katika masuala mengine pia ya kijamii pale inapowezekana.

UAP ni kampuni ya bima yenye makao makuu yake jijini Dar es Salaam. UAP ina matawi 9 yanayopatikana katika mikoa mbalimbali hapa nchini kama vile Dar Es Salaam, Arusha, Mbeya, Mwanza, Dodoma, Kahama, Zanzibar, Morogoro na Mtwara.

No comments