Breaking News

TBS KANDA YA MAGHARIBI YAWATAKA WAZALISHAJI KUTHIBITISHA UBORA WA BIDHAA KUSHIKA SOKO LA AFRIKA MASHARIKI

   Na Mwandishi Wetu.

SHIRIKA la Viwango Tanzania (TBS) Kanda ya Magharibi limetoa wito kwa wazalishaji, wafanyabiashara pamoja na wananchi kutumia fursa za kuthibitisha ubora wa bidhaa zao ili kuweza kupata nafasi ya kushiriki katika soko linalokua kwa kasi la Afrika Mashariki. 

 

Akizungumza katika maonesho ya Lake Tanganyika Expo 2026 ambayo yalianza Septemba 16 hadi 22 yanayofanyika katika viwanja vya Community Center mkoani Kigoma, Meneja wa TBS Kanda ya Magharibi, Hamisi Simon Seleleko alisema kuwa shirika hilo linahudumia mikoa mitatu ambayo ni Kigoma, Katavi, na Tabora.  

Alisema kuwa lengo kuu la kushiriki katika maonnesho hayo ni kutangaza huduma mbalimbali zinazotolewa na TBS na kuwaonesha wajasiriamali na wazalishaji fursa zinazopatikana kupitia udhibitisho wa ubora wa bidhaa.  

 

"Uthibitishaji wa ubora unampa mzalishaji fursa ya kuingiza bidhaa yake kwenye soko la ndani na nchi wanachama wa Afrika Mashariki, ambalo hadi sasa linajumuisha nchi nane," alisema.  

Aidha alisema katika maonesho hayo, TBS imeweka dawati maalum la kutoa huduma za papo kwa papo kwa wananchi na wadau wanaotembelea banda lao. 

Alitaja huduma hizo kuwa ni pamoja na 

usajili wa bidhaa kutoa elimu na usajili wa bidhaa za chakula na vipodozi. 

Alisema usajili huo ni kigezo cha msingi kinachoonesha kuwa bidhaa hizo ni salama kwa matumizi ya jamii.  

Pia alisema wanatoa elimu juu ya bidhaa zilizopigwa marufuku na kuwaonesha wananchi na wafanyabiashara mifano ya vipodozi na bidhaa zisizokidhi viwango au vyenye viambata hatari ambavyo vimepigwa marufuku ili kuepuka madhara ya kiafya.  

Aidha alitoa wito kwa wazalishaji wote kutumia fursa ya maonyesho hayo kuwasilisha maombi yao kupitia mtandao na kukidhi vigezo ili maofisa wa TBS waweze kukagua maeneo yao ya uzalishaji, kupima bidhaa, na kuwapatia leseni ya kutumia alama ya ubora.  

Pia, alitumia fursa hiyo kuwakaribisha wafanyabiashara wa chakula na vipodozi kufika katika banda la TBS ili kupata usaidizi wa ukaguzi na usajili katika kipindi hiki cha maonyesho.









No comments