Breaking News

NANE NANE 2026: TBS YATIA MKAZO UBORA WA BIDHAA KUSHINDANA SOKO LA AFRIKA

Na Mwandishi Wetu - Morogoro

Katika kipindi ambacho Maonesho ya Nane Nane 2026 yanaendelea nchini, Shirika la Viwango Tanzania (TBS) limewataka wazalishaji wa bidhaa nchini kuhakikisha bidhaa zao zinathibitishwa ubora, hatua inayolenga kuwawezesha kupata masoko mapana ndani na nje ya Tanzania.

Wito huo umetolewa wakati wa Maonesho ya Nane Nane Kanda ya Mashariki yanayofanyika mkoani Morogoro, ambapo TBS imeeleza kuwa uthibitishaji wa ubora ni moja ya nyenzo muhimu kwa mzalishaji kuondokana na vikwazo vya kibiashara na kuongeza uaminifu wa bidhaa katika masoko ya kitaifa, kikanda na kimataifa.

                 

Akizungumza katika maonesho hayo, Meneja wa TBS Kanda ya Dar es Salaam, Bi. Noor Meghji, amesema taasisi hiyo ipo kwa ajili ya kuwawezesha wazalishaji na wajasiriamali kuhakikisha bidhaa zao zinafikia viwango vinavyokubalika, hivyo kuongeza ushindani wao katika masoko.

                  

Amesema hatua hiyo inaendana na dhima ya Nane Nane 2026 inayosisitiza matumizi ya taarifa za masoko, kuongeza tija, kuongeza thamani ya bidhaa pamoja na kukuza ushindani katika masoko ya kimataifa.

Kwa mujibu wa Bi. Meghji, TBS kwa kushirikiana na Shirika la Viwango la Afrika (ARSO), imezindua Alama ya Ubora ya Afrika, ambayo inalenga kusaidia bidhaa zinazokidhi viwango kupenya katika masoko mapana ya Afrika, ikiwemo Eneo Huru la Biashara Barani Afrika (AfCFTA).

“Tunatoa wito kwa wazalishaji wa bidhaa nchini kuthibitisha ubora wa bidhaa wanazozalisha, kwani kwa kufanya hivyo wanaongeza na kutanua wigo wa masoko ya bidhaa zao,” amesema Bi. Meghji.

Aidha, TBS imewahamasisha wajasiriamali kutumia fursa ya uthibitishaji wa ubora inayotolewa kwa gharama za Serikali, hatua ambayo kwa mujibu wa shirika hilo itawasaidia wazalishaji kuondokana na baadhi ya vikwazo vinavyoweza kuzuia bidhaa zao kuingia katika masoko mbalimbali.

Bi. Meghji amesema bidhaa zinazokidhi viwango na kuthibitishwa na TBS zina nafasi kubwa zaidi ya kuaminika katika masoko ya kikanda, huku fursa ya AfCFTA ikifungua wigo mpana zaidi kwa wazalishaji wa Tanzania.

Kwa upande wake, Meneja wa TBS Kanda ya Mashariki, Mhandisi Cyril Kimario, amewataka wananchi kuwa makini wakati wa kununua bidhaa kwa kuhakikisha wanachagua bidhaa zilizothibitishwa ubora na kusoma taarifa zilizowekwa kwenye vifungashio.

Amesema kufanya hivyo kutamsaidia mlaji kuwa na uhakika wa bidhaa anayoinunua na kulinda afya pamoja na maslahi yake kiuchumi.

“Kununua bidhaa zilizothibitishwa ubora wake humhakikishia mwananchi usalama wa afya yake pamoja na uchumi wake, kwani anakuwa amepata kitu bora chenye thamani katika afya na uchumi,” amesema Mhandisi Kimario.

Maonesho ya Nane Nane 2026 yanafanyika kuanzia Agosti 1 hadi 8 na yamebeba msisitizo wa kukuza ubunifu, biashara na ushindani katika mnyororo wa thamani wa kilimo. Kilele cha maadhimisho hayo ni Agosti 8, ambapo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika hafla ya wakulima, wafugaji na ufungaji wa maonesho.

Kwa wazalishaji, ujumbe kutoka TBS ni mmoja: bidhaa bora si kinga ya soko la ndani pekee, bali ni tiketi ya kushindana katika soko la Afrika na dunia.

               

No comments