TBS WASHIRIKI MAONESHO YA BAIOTEKNOLOJIA COSTECH - DAR ES SALAAM
Na Mwandishi Wetu.
Shirika la Viwango Tanzania (TBS) limeshiriki katika Maonesho ya Baioteknolojia yaliyofanyika katika Ofisi za Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH), jijini Dar es Salaam, yakilenga kutoa elimu kwa wananchi kuhusu umuhimu wa viwango.
Akizungumza katika maonesho hayo, Februari 12, 2026 Jijini Dar es Salaam, Afisa Mdhibiti Ubora wa TBS, Neema Kirway, amesema shirika hilo limeshiriki kikamilifu ili kuongeza uelewa wa wananchi kuhusu jukumu la TBS katika kudhibiti ubora na usalama wa chakula pamoja na bidhaa nyingine.
Amesema TBS tayari imeanzisha viwango 74 vya Baioteknolojia, hatua inayolenga kulinda afya, usalama na maslahi ya Mtanzania.
“Kupitia viwango hivi, TBS itahakikisha kuwa bidhaa zote za Biotechnology zinakidhi ubora na usalama kabla ya kumfikia mtumiaji,” amesema Kirway.
Aidha, amebainisha kuwa shirika hilo liko katika mchakato wa kuandaa viwango vingine vya Biotechnology, ambavyo vipo katika hatua za mwisho kabla ya kutangazwa rasmi.
Kirway ametoa rai kwa wadau na wananchi kufahamu kuwa viwango hivyo vinapatikana na vinauzwa katika Makao Makuu ya TBS.
Amesisitiza kuwa TBS itaendelea kusimamia kikamilifu utekelezaji wa viwango ili kuhakikisha bidhaa zote zinazosajiliwa na kupitishwa na shirika hilo ni salama kwa matumizi ya binadamu.
Katika ufafanuzi wake, Kirway amesema teknolojia ya Biotechnology ina mchango mkubwa katika sekta mbalimbali ikiwemo afya, kilimo, viwanda na usalama wa chakula.
“Elimu iliyotolewa katika maonesho haya inasisitiza umuhimu wa wanasayansi kushirikiana, kubadilishana uzoefu na kuimarisha matumizi ya teknolojia na Biotechnology kwa maendeleo ya taifa,” ameongeza.
Kauli mbiu ya maonesho hayo ilikuwa: “Biotechnology Kuimarisha Usalama wa Chakula na Maendeleo ya Jamii na Uchumi.”










No comments