Breaking News

MIXX BY YAS YASHIRIKIANA NA UBX, SCCULT KURAHISISHA HUDUMA ZA MIKOPO NA MICHANGO KWA SACCOs NCHINI

 Na Mwandishi Wetu.

Dar es Salaam, 22 Mei 2025 – Mixx by Yas imeingia katika ushirikiano wa kimkakati na Kampuni ya UBX na Chama Kikuu cha Ushirika wa Akiba na Mikopo Tanzania (SCCULT), kama mshirika rasmi wa malipo kidijitali kwa wanachama wa chama hicho Tanzania nzima.

Kupitia ushirikiano huu, wanachama wa SACCOs wataweza kuweka akiba na kufanya marejesho ya mikopo kwa njia rahisi na salama kwa kutumia Mixx by Yas, bila kujali mtandao wa simu wanaotumia. Mfumo huu mpya unalenga kuboresha upatikanaji wa huduma za kifedha hasa kwa Watanzania waliopo maeneo ya pembezoni.

Akizungumza wakati wa hafla ya utiaji saini wa makubaliano hayo, Dkt. Khadija Kishimba mwakilishi kutoka Benki Kuu ya Tanzania akimuwakilisha Mkurugenzi wa Ustawi na Huduma Jumuishi za Fedha wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Bw. Kennedy Komba, alisema:

“Hii ni hatua kubwa kuelekea katika kujenga mfumo jumuishi wa kifedha kwa Watanzania wote. SACCOs zina mchango mkubwa katika kuwafikia wananchi walioko maeneo yenye changamoto za upatikanaji wa huduma rasmi za kifedha. Ushirikiano kati ya Mixx by Yas na UBX ni mfano bora wa jinsi sekta binafsi inavyoweza kusaidia kufanikisha ajenda ya kitaifa ya ujumuishaji wa kifedha.”

Kwa upande wake, Afisa Mtendaji Mkuu wa Mixx by Yas, Bi. Angelica Pesha, alisema kuwa ushirikiano huu unalenga kuimarisha ujumuishaji wa kifedha kwa wanachama wa SACCOs kwa kutumia teknolojia ya simu za mkononi. Kupitia suluhisho hili la kidigitali, wanachama wa SACCOs wataweza kuweka akiba, kurejesha mikopo na kupata huduma nyingine za kifedha bila kutembelea ofisi wala kujaza makaratasi.

"Mixx tunaamini kuwa kila Mtanzania, popote alipo, anapaswa kupata huduma za kifedha kwa njia rahisi, salama na ya kisasa. Ushirikiano huu ni hatua ya mabadiliko, hasa ikizingatiwa kuwa chini ya asilimia 5 ya SACCOs ndizo zinazotumia teknolojia ya simu za mkononi kutoa huduma leo hii," alisema.

Takwimu za Ripoti ya Finscope ya mwaka 2023 zinaonyesha kuwa ni asilimia 2 tu ya Watanzania ndio wanaotumia huduma za SACCOs, licha ya mchango wake mkubwa kwa jamii za mijini na vijijini. Ushirikiano huu wa Mixx, UBX na SCCULT unalenga kubadili hali hiyo na kuwezesha wanachama wa SACCOs kupata huduma kwa urahisi kupitia simu zao.

Mkurugenzi Mtendaji wa UBX, Bw. Seronga Wangwe alisema:

“Kupitia mfumo huu, SACCOs zitakuwa na uwezo wa kutoa mikopo papo kwa papo huku zikihakikisha uwazi na usahihi wa takwimu. Hii ni hatua muhimu katika kujenga uaminifu baina ya SACCOs na wanachama wao.”

Mfumo huu mpya, unatarajiwa kuanza kutumika rasmi katika robo ya tatu ya mwaka 2025 kwa SACCOs zote zilizo chini ya SCCULT. Lengo kuu ni kupunguza ucheleweshaji wa huduma, makosa ya kibinadamu, utegemezi wa makaratasi, na kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma za kifedha vijijini na mijini.











No comments