Breaking News

WFP yatembelea makao makuu ya Kampuni ya Meli Tanzania, yajionea utendaji kazi wa MV Umoja


Na Mwandishi Wetu, Mwanza


Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula Duniani (World Food Programme -WFP) limesema litaendeleza mashirikiano na Kampuni ya Meli Tanzania (TASHICO) katika eneo la usafirisaji wa shehena ya vyakula kutoka Bandari ya Dar es Salaam na Mwanza mpaka Sudan ya Kusini.

Wawakilishi wa WFP kutoka makao makuu yalipo Roma, Italia wametembelea makao makuu ya TASHICO jijini Mwanza ili kuweza kufanya tathmini ya mashirikano waliyoanzisha takribani miaka kumi.

Ugeni huo kutoka WFP ulipata fursa ya kuweza kutembelea meli ya MV Umoja, meli ambayo alikuwa ikitumika kusafirisha shehena ya vyakula kutoka Bandari ya Mwanza nchini Tanzania kwenda Sudani ya Kusini kupitia Uganda.

Akiongea mara baada ya kutembelea meli ya MV Umoja katika Bandari ya Mwanza jana , Afisa Ufuatiliaji na Tathmini wa WFP Sala Maharenovic amesema kuwa wamekuja kufanya tathmini ya mashirikiano waliyoingia na Kampuni ya Meli Tanzania wakati huo ikijulikana kama Kampuni ya Huduma za Meli (MSCL), amesema kuwa mashirikiano walioanzisha yamekuwa yenye tija ambapo wamekuja kufanya tathmini ya mashirikiano  kati yao na wadau wao ambapo mmoja ya wadau wakubwa akiwa ni TASHICO.  


“Mazungumzo haya ya pamoja ni muhimu katika kupata tathmini ya kina na kuelewa ni mahitaji gani yanatohitajika sasa ili kuboresha zaidi mahusiano yetu kwa pamoja WFP na Kampuni ya Meli Tanzania,” alisema Afisa huyo mwandamizi wa WFP.

Baada ya kupokea ugeni kutoka makaomakuu ya WFP, Mkurugenzi Mtendaji wa TASHICO Eric Hamissi amesema: “Nimefurahi kupokea ujumbe huu wa WFP ambao wamekuja kutembelea katika makao makuu ya Kampuni yetu, hii inaendelea kukuza mahusiano mema tuliyoaanzisha. TASHICO imekuwa na uhusiano wa  karibu sana wa kikazi na WFP kwa miaka mingi. Nakumbuka wakati huo meli yetu kubwa ya mizigo ya MV. Umoja ilikuwa ikifanya kazi kwa kusuasua lakini tuliweza kupata shehena nyingi ya mizigo kutoka kwa wadau wetu hawa kutoka Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulika na Mpango wa Chakula Duniani.”


Aliongezea: “Ujio wa timu hii ni mwanzo wa kuona namna ya kurejesha usafirishaji shehena ya mizigo toka kwao. Meli ya MV. Umoja ilisimama kufanya kazi mwaka 2019 na  serikali  ilitoa hela  bilioni 19.5 mwaka 2021  kwa ajili ya ukarabati mkubwa na hatimaye meli imerejea tayari.” 


Mkuu wa Kitengo cha usafirishaji na ugavi wa WFP Tanzania Mamoud Mabuyu amesema: “Tumekuja hapa na ugeni kutoka Makao Makuu ya Shirika letu yaliyopo Roma, Italia ambapo wamekuja kufanya tathmini kuangalia ni jinsi gani ambavyo tunafanya kazi na washirika wetu kwenye eneola usafirishaji abapo TASHICO ni mmoja wa washirika wetu wakubwa.”

“Ugeni huu umekuja baada ya miaka kumi ambayo tumefanya kazi pamoja na TASHICO hivyo tathmini itaweka wazi ni kiasi gani mahusiano yetu yamekuwa na faida kwetu sisi na kwa mashirika ambayo tunafanya nayo kazi na nchi kwa ujumla, na vile vile kupendekeza nini cha kufanya baaa ya hapa,” alimalizia afisa huyo kutoka WFP Tanzania.


Naye Eugenia Punjila, Afisa Masoko Mkuu wa TASHICO amesema kuwa WFP wamekuwa wakisafirisha shehena ya chakula na mahitaji mengine ya msaada kupitia meli kwenda nchini Sudani ya Kusini kupitia Uganda. 

“Tunaishukuru Serikali kwa kuendelea kuwekeza zaidi kwa TASHICO kwa wakati huu ambapo tunakabiliana na shehena kubwa,” alisema.


Naye, Nahodha mkogwe wa meli ya MV Umoja Bembele Samson N'gwita amesema hivi sasa kuwa kuna mabadiliko makubwa baada ya ukarabati mkubwa uliofanyika kwenye meli hii ya MV Umoja tofauti na ilivyokuwa miaka kumi iliyoita. 

Hata hivyo, TASHICO ni taasisi ya serikali ambayo ilianza kazi zake mwaka 1961 chini ya jina la TRC Marine Division, ikiwa na ari kubwa ya kuendeleza sekta ya meli nchini na hadi sasa imeweza kutekeleza miradi kadhaa madhubuti.

Miradi hiyo pamoja na mingine ni pamoja na ile iliyojikita katika ukarabati wa meli zilizochakaa, ujenzi wa meli mpya pamoja na kuboresha usafiri wa majini nchini Tanzania, hasa katika maeneo muhimu yenye wakazi wengi wa maziwa ya Victoria, Tanganyika na Nyasa.


Mwisho

No comments