Mazars Wiscon Associates yabadili chapa yake Rasmi
Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya Mazars Tanzania inayotoa huduma za ushauri wa kodi, ukaguzi wa mahesabu na ushauri wa mambo ya fedha, Witness Shilekirwa (kushoto), na mmoja wa washirika wa kampuni hiyo, Ipyana Lazaro wakiwa katika mkutano na waandishi wa habari Dar es Salaam leo wakati wakitangaza kuzindua chapa na jina lao jipya ambalo awali waliitwa Mazars Wiscon Associates.
Dar es Salaam, 21 Oktoba 2020: Mazars, kampuni ya kimataifa inayotoa huduma za ushauri wa kodi, ukaguzi wa mahesabu na ushauri wa mambo ya fedha. Leo tumefungua ukurasa mpya kote ulimwenguni katika nchi zaidi ya 90 ikiashiria hatua muhimu katika mageuzi ya kampuni hii.
Akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari, mmoja wa wabia washirika wa Mazars Group Bw. Ipyana Lazaro alisema wanafuraha kubwa kuwa ni washirika wa kampuni ya ukaguzi wa mahesabu iliyoenea ulimwenguni kote.
“Sisi kama washirika wa Mazars, tunajivunia sana chapa yetu mpya. Mazars imekuwepo Tanzania tangu mwaka 2017, ikihudumia wateja wa aina tofauti, wakubwa kwa wadogo. Chapa yetu mpya inatutambulisha na kutuweka kwenye mtazamo tofauti kitaifa na kimataifa, na kuendana na mabadiliko haya, leo tumebadili jina rasmi kutoka Mazars Wiscon Associates na kuwa Mazars Tanzania.”, alisema.
Mabadiliko haya ni miongoni mwa malengo ya Mazars kuleta mtazamo tofauti katika soko la biashara ya ukaguzi wa mahesabu, ushauri wa kodi, maswala ya fedha na uchumi kiujumla, na inathibitisha dhamira yake ya kujenga ulimwengu wa haki, ustawi na uendelevu.
Naye Mwenyekiti na Mkurugenzi Mtendaji wa Mazars Group Bw. Hervé Hélias, katika ujumbe wa salamu zake alisema ana furaha sana kuzindua kitambulisho kipya baada ya miaka miwili ya mashauriano ya kina na mapana na washirika, wafanyikazi, wateja na wadau.
“Uzinduzi huu wa chapa yetu mpya unaonesha sisi ni nani leo na kuthibitisha matarajio yetu kwa aina ya kampuni tunayotaka kuwa katika siku zijazo. Sisi ni timu moja iliyounganishwa kote ulimwenguni, na kiwango cha kuhudumia wateja wakubwa wa kimataifa na ni wepesi wa katika ubunifu na katika kuleta mabadiliko.”
Bw. Helias aliongeza kuwa katika kila nchi ambayo kampuni ya Mazars inapofanya kazi, washirika na wafanyakazi huchanganya uelewa wa kitamaduni wa nchi husika na mtazamo wa kimataifa, ikihudumia wateja wa aina mbalimbali kwa ushirikiano wa kweli, ambao unawapa ujasiri katika biashara zao na kuwasaidia kufanikisha azma zao.
Chapa mpya inaashiria na inatambua mageuzi makubwa yaliyofanywa na Mazars kimataifa, ambapo kwa sasa Mazars ina uwepo katika nchi zaidi ya 90, na ina wataalam zaidi ya 25,000 duniani kote. Pia Mazars kupitia umoja unaojulikana kama “Mazars North America Alliance”, umeleta wataalamu wa ziada 16,000 wanaotoa huduma kwa wateja wa makampuni ya Amerika na Canada. Kwa jumla tuna wataalamu zaidi ya 40,000 wanaosaidia wateja wa Mazars ulimwenguni kote.
Hervé Hélias akiendelea kutoa maoni yake alisema "Kwa miaka 75, kanuni zetu zinazotuongoza hazijabadilika, lakini kampuni yetu imebadilika. Tumekua mara dufu katika miaka kumi iliyopita na tumejitofautisha katika kuhudumia wateja wetu."
Mazars tunaendelea kuwekeza kwenye idara ya ukaguzi (Audit) – kwa kufundisha na kutoa wataalam (expertise), kuwekeza kwenye teknolojia na udhibiti wa ubora (quality control). Idara hii inahitaji kuwekeza kwenye utaalam na ubunifu.
“Ili kuendana na matakwa na mabadiliko makubwa yanayoendelea duniani kote. Tumejitahidi sana kuwekeza kwenye ubunifu, usalama wa mifumo na udhibiti wa ubora ili kuendelea kuwa kwenye soko la leo” alimalizia Bw. Helias.
- Sasa yapanua wigo wake katika nchi zaidi ya 90 ili kuleta mafanikio na mtazamo tofauti katika kazi ya ukaguzi, kutoa huduma za kodi na ushauri kwa ujumla
- Mabadiliko ya chapa yanathibitisha mkakati wa kujenga ulimwengu wa haki na mafanikio
No comments