Sanlam yachangia TZS 172,500,000 kuunga mkono mapambano dhidi ya ugonjwa wa COVID-19 nchini
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu (wa pili kushoto), akipokea mfano wa hundi ya shs 172,500,000 zilizotolewa na Kampuni ya Bima ya Sanlam Life Insurance na Sanlam General Insurance kusaidia juhudi za serikali katika kupambama wa ugonjwa wa homa kali ya mapafu unaosababishwa na virusi vya Corona (covid-19). Hafla ya makabidhiano ilifanyika ofisini kwa Waziri Mkuu, jijini Dar es Salaam hivi karibuni. Kutoka kushoto ni; Mkuu wa Kitengo cha Rasilimali Watu wa Sanlam Life, Charles Mbaga, Mwenyekiti wa Bodi wa Sanlam, Balozi Dk. Matern Lumbanga, Ofisa Mtendaji Mkuu wa Sanlam Kanda ya Afrika Mashariki, Julius Magabe na Ofisa Mtendaji Mkuu wa Sanlam Genral Tanzania, Gift Noko.
Na Mwandishi Wetu.
WAKATI maambukizi ya virusi vya Corona Tanzania yakiongezeka, Sanlam Life Insurance na Sanlam General Insurance ambayo ni makampuni tanzu ya Sanlam Group yanayoongoza kwa kutoa huduma za bima nchini, yameungana na Watanzania wengine kuchangia Shilingi 172,500,000 katika juhudi za kuupiga vita ugonjwa wa COVID-19.
Fedha hizo zimekabidhiwa rasmi kwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Kassim Majaliwa ambaye pia ni Mwenyekiti wa Taifa wa Kamati ya kukabiliana na maambukizi ya COVID-19 ambapo Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu, amepokea msaada huo kwa niaba ya Waziri Mkuu.
Fedha zilizotolewa zinalenga kusaidia upatikanaji wa vifaa kinga na vifaa tiba husika kwa wahudumu wa afya, wagonjwa na jamii kwa ujumla.
Akizungumza katika hafla fupi ya kukabidhi mchango huo, Ofisa Mtendaji Mkuu wa Sanlam – Kanda ya Afrika Mashariki, Bwana Julius Magabe amesema kampuni ya Sanlam imeguswa na janga hili la kidunia na kuona ni busara kuunga mkono juhudi za serikali katika mapambano haya na kutoa mchango huu.
“Makampuni ya bima ya Sanlam nchini yakiwa sehemu ya jamii, yanatambua kuwa ni wajibu muhimu kama taasisi kuwa sehemu ya jitihada hizi za kuhakikisha usalama wa afya ya jamii ambayo inatuzunguka,” amesema Bwana Magabe.
Bwana Magabe alieleza zaidi kuwa kama Sanlam Group na kampuni zake zilizopo Tanzania (Sanlam Life Insurance na Sanlam General Insurance), wanaimani kuwa elimu kwa jamii kuhusiana na janga hili la COVID-19 inatakiwa kuendelea kutiliwa mkazo, na kwamba michango ya wadau mbalimbali wa maendeleo itakuwa na msaada mkubwa kwenye hili, kusaidia watu kubadili tabia kama inavyoelekezwa na wataalamu wa afya, ili jamii ya Watanzania ibaki salama.
Kwa niaba ya Waziri Mkuu, Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu ameushukuru uongozi wa Sanlam kwa kuunga mkono juhudi za serikali katika wakati huu muhimu.
“Msaada huu umekuja katika wakati muafaka kwetu na hivyo, pamoja na shukurani, tunatoa wito kwa kampuni, taasisi na wafanyabiashara binafsi kuendelea kuisaidia serikali kwa hali na mali katika mapambano haya. Tunaahidi hatutawaangusha,” amesema Ummy.
Pamoja na kuchangia mapambano dhidi ya COVID-19, makampuni ya Sanlam yamechukua hatua stahiki pahala pa kazi kuhakikisha usalama wa wateja na wafanyakazi unalindwa.
No comments